Shule ya Imam Zaynul Aabidin (a.s) Yatoa Msaada wa Mifugo kwa Waislamu wa Bujumbura - Burundi +Picha
Msaada huu unatarajiwa kusaidia familia kadhaa katika Jiji la Bujumbura, hususan zile zenye uhitaji, na kuleta mfano mzuri wa umoja, ukarimu na heshima baina ya Waislamu wa Madhehebu mbalimbali, kama ilivyofundishwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Ahlul-Bayt (a.s).
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-, Bujumbura, Burundi - Jumapili, 5 Oktoba 2025 - Katika tukio lenye kuonyesha roho ya mshikamano na ukarimu wa Kiislamu, Shule ya Imam Zaynul Aabidin (a.s) kwa niaba ya Taasisi ya Kimataifa ya Jamiat Al-Mustafa (s) Dar-es-salaam - Tanzania, imetoa msaada wa Mbuzi na Kondoo 20 kwa Sheikh Asadullah Omar, ambaye ni Mkuu wa Jiji la Bujumbura na Mwakilishi rasmi wa Mufti wa Waislamu wa Sunni-Shafi‘i nchini Burundi.
Msaada huu umetolewa kama sehemu ya juhudi za Taasisi ya Jamiat Al-Mustafa (s) katika kuimarisha undugu wa Kiislamu, kusaidia jamii zenye uhitaji na kukuza uhusiano wa kidini na kijamii baina ya Waislamu wa Madhehebu mbalimbali.
Kwa upande wake, Mufti Mkuu wa Sunni-Shafi‘i nchini Burundi, kupitia Mwakilishi wake Sheikh Asadullah Omar, alitoa shukrani za dhati na pongezi kwa uongozi wa Jamiat Al-Mustafa (s), akisisitiza kuwa msaada huo ni kielelezo cha wazi cha upendo, amani, na ushirikiano wa Kiislamu.
Aidha, Mufti alitoa shukrani maalumu kwa Dkt. Ali Taqavi, ambaye ni Mwakilishi wa Taasisi ya Jamiat Al-Mustafa (s) katika nchi za Tanzania, Burundi na Malawi, akisema kwamba juhudi na bidii zake katika kueneza elimu, Maarifa, kusaidia jamii, na kuimarisha uhusiano wa Kiislamu haziwezi kuelezewa kwa maneno.
Msaada huu unatarajiwa kusaidia familia kadhaa katika Jiji la Bujumbura, hususan zile zenye uhitaji, na kuleta mfano mzuri wa umoja, ukarimu na heshima baina ya Waislamu wa Madhehebu mbalimbali, kama ilivyofundishwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Ahlul-Bayt (a.s).
Your Comment